Tuesday, 24 May 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumuwakilisha tena Rais Magufuli katika mkutano huu.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliondoka nchini jana kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria mkutano wa 51 wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika utakaofanyika kesho.

Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais John Magufuli ikiwa ni mara yake ya tatu kumuwakilisha mkuu huyo wa nchi.

Mara ya kwanza alimuwakilisha nchini Botswana katika mkutano wa Sadc na mapema mwezi huu alimuwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi wa kujadili mapambano dhidi ya rushwa London, Uingereza.

Mkutano huo wa Zambia ambao utafunguliwa na Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya nishati na mabadiliko ya tabianchi. Pia, mkutano huo utahudhuriwa na marais Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Nigeria itawakilishwa na Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji ikiwakilishwa na Waziri Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.

Watu maarufu waliothibitisha kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo-Iweala na Tony Elumelu.

Mkutano huo utakaofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi utakuwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka nchi 26 ambazo si za bara la Afrika, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Wengine watakaohudhuria ni mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na wataalamu kutoka vyuo vikuu.

Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, wachumi kadhaa na wataalamu wa sekta ya fedha.

No comments:

Post a Comment