Friday, 24 June 2016

Hii ndio Ripoti iliyotolewa na NEC kuhusu uchaguzi mkuu 2015 na kukabidhiwa Rais Magufuli.



Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva amekabidhi taarifa hiyo kwa Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zuberi Ali Maulid, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Wengine ni Mawaziri Wakuu wastaafu Dkt. Salim Ahamed Salim na Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Mhe. Jecha Salum Jecha, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamishna wa tume ya uchaguzi, Msajili wa vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini na Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa taarifa hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendesha uchaguzi vizuri na kuhakikisha watanzania wanatumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Rais Magufuli pia amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika katika hali ya amani na usalama na nchi inaendelea kuwa katika amani na utulivu baada ya uchaguzi.
Dkt. Magufuli amewapongeza na kuwashukuru viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, waangalizi mbalimbali wa uchaguzi, vyombo vya habari, mashirika ya ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa walioutoa wakati wa mchakati wa uchaguzi mkuu na ameomba ushirikiano huo uendelee hata katika uchaguzi mwingine.

Hata hivyo, Rais Magufuli amesema kwa sasa uchaguzi umekwisha na ametaka watanzania wote wajielekeze kufanya kazi na kwamba serikali yake haitavumilia vitendo vyovyote vitakavyoathiri utekelezaji wa ahadi zake kwa watanzania katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

"Yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano, nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kuyatekeleza hayo niliyoyaahidi, nasema nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kuyatekeleza hayo niliyoyaahidi katika kipindi cha miaka mitano, niwaombe wanasiasa wenzangu, ushindani wa sasa hivi wa vyama vya siasa unatakiwa uweke nguvu zaidi kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi, kama ni kwa madiwani wakapeleke hoja kwa nguvu sana kwenye maeneo yao, kama ni wabunge wakazungumze kwa nguvu zote bungeni.

"Tumeamua kufanya kazi tutashirikiana na vyama vyote katika kuhakikisha tunatatua kero za wananchi, na huo ndio wajibu wangu, na hili nitalisimamia kwa nguvu zangu zote" Amesema Rais Magufuli

Kuhusu mchakato wa katika mpya Dkt. Magufuli ameipongeza kazi kubwa iliyofanywa katika uongozi wa awamu ya nne na ameahidi kuwa serikali yake itaendeleza mchakato huo kutoka pale ulipoishia.

Awali akitoa taarifa ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema uchaguzi huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa ambapo jumla ya watanzania walioandikishwa kupiga kura walikuwa 23,161,440 sawa na asilimia 96.9 ya makusudio ya kuandikisha watanzania 23,901,471 na kwamba watanzania 15,596,110 sawa na asimilia 67.34 walijitokeza kupiga kura.

No comments:

Post a Comment