Thursday, 23 June 2016

Rais Kagame kufungua Maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba).



Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini tarehe 01 Julai 2016 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mhe. Dkt, John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


Akiwa nchini Mheshimiwa Rais Kagame atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli na baadaye kwa pamoja viongozi hao watashuhudia uwekaji saini wa Makubaliano ya Pamoja (MoUs) baina ya Tanzania na Rwanda katika sekta mbalimbali za ushirikiano. 

Aidha, Mheshimiwa Kagame atashiriki dhifa rasmi ya kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Magufuli .
Mchana wa tarehe 1 Julai, 2016 Mheshimiwa Rais Kagame akiambatana na mwenyeji wake atahudhuria maonesho ya 40 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kama Mgeni Rasmi kwa ajili ya kuyafungu.

Ziara hiyo ya Mheshimiwa Kagame inafuatia ziara yenye mafanikio aliyofanya Mhe. Dkt. John Pombe Jospeh Magufuli nchini Rwanda mwezi Aprili 2016. Ziara hiyo ni ishara nyingine ya kuimarika kwa mahusiano baina ya nchi hizi mbili.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 23 Juni 2016

No comments:

Post a Comment