Monday 13 June 2016

Wachambuzi wazungumza haya kuhusu wabunge wanaopinga kukatwa kodi katika kiinua mgongo chao.

WABUNGE wanaopinga kiinua mgongo chao wanachopata baada ya miaka mitano kutozwa kodi, wamenyooshewa vidole na kuambiwa wanakwepa majukumu yao ya kuwajibika na kujiaibisha kwa wananchi.


Miongoni mwa watu waliozungumzia kitendo hicho, wamesema wabunge wanaopinga kukatwa kodi, wanajiaibisha kwa wananchi; ambao licha ya wengi kuwa na kipato cha chini, wanalipa kodi. Katika kuunga mkono mapendekezo hayo ya serikali kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge, yaliyomo kwenye hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 , baadhi ya watu wamekwenda mbali na kushauri pia ruzuku za vyama vya siasa zianze kukatwa kodi kwa ajili ya kuongeza mapato.

Wabunge wajipime Wamesema wabunge wana wajibu wa kujipima kama michango yao kwa Watanzania na serikali inaishia kuongea bungeni au pia uchangiaji wa kodi, ambazo kila Mtanzania anachangia kulingana na nafasi yake. Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, watu wa kada mbalimbali walisema kila mwananchi bila kujali wadhifa wake, analo jukumu la kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema jukumu la raia mwema ni kulipa kodi kusaidia serikali yake . Alisema wabunge ni miongoni mwa raia hao, ambao wanapaswa kutambua kwamba hawapaswi kukwepa jukumu hilo. “Mbunge ni kama raia wengine ambao wanatakiwa kuchangia nchi yao; Tena kiongozi mwenye sifa ni yule anayechangia nchi yake, anatembea kifua mbele kwa kuchangia, wewe mbunge usiyechangia ni kiongozi wa aina gani?” Alihoji Dk Bana.

Ruzuku za vyama Aidha, Dk Bana alisema pamoja na wabunge kukatwa kodi, serikali iangalie pia namna ya kukata kodi katika ruzuku ambazo vyama vya siasa hupata ambavyo kwa sasa hawakatwi. “Serikali pia iangalie namna ya kukata kodi katika vyama hivi ambavyo kazi yao kubwa fedha hizo ni kuandaa mikutano ambayo ni vurugu tupu na kesi mahakamani kila kukicha,” alisema Dk Bana.

Hata hivyo, mhadhiri huyo wa chuo kikuu alisema, wabunge wanachotakiwa kufanya, ni kuomba majadiliano na serikali kiasi ambacho wanaona kinapaswa kukatwa kwenye kiinua mgongo chao. Alisema si sahihi kukataa kukatwa kodi wakati Watanzania wa hali ya chini wanakatwa kodi. Alisisitiza kuwa wabunge wanapaswa kujipima kuwa michango yao kwa Watanzania na serikali ni michango yao ya maneno bungeni au pia katika kodi ambazo kila Mtanzania anapaswa kulipa nao wanachangia.

Alishauri wabunge waelimishwe juu ya suala hilo huku akisisitiza kuwa ni jambo lisilowezekana kwa wanasiasa hao ambao hupanga mambo mbalimbali ikiwemo sheria za kodi, wakati wao wenyewe hawataki kuzitii. “Huu utakuwa ni uongozi mbovu ambao wabunge wanauonesha, hii ni mipango ya serikali katika kukusanya kodi hivyo na wabunge wanapaswa kushirikiana na serikali kuwaletea wananchi maendeleo ambayo yanapatikana baada ya kukusanywa kodi,” alisema Bana na kupongeza serikali kwa hatua hiyo.

Wanajiaibisha Kwa upande wake, Mhadhini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema wabunge wanapaswa kutambua kwamba serikali imepania kukusanya kodi hivyo hawapaswi kukataa au kupingana nayo. Mkumbo ambaye pia ni Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, alisema wabunge wanaopinga kukatwa kodi wanajiaibisha kwa wananchi kwani wananchi wa kipato cha chini wanalipa kodi.
“Katika kujenga nchi mchango wako unakuwa katika kulipa kodi na mfano huo unatakiwa kuoneshwa na viongozi wenyewe ambao ni pamoja na wabunge,” alisema Mkumbo.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment