MAHAKAMA Maalumu ya kushughulikia Makosa ya Rushwa na Ufisadi, inaanza rasmi leo Julai mosi.
Pamoja na kuanza kwa mahakama hiyo, serikali imeanza mchakato kuifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ya Mwaka 2007 ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa sasa.
Mahakama hiyo iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na imo katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi, itaimarisha zaidi taasisi za uwajibikaji zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa.
Ahadi hiyo ambayo inatimizwa ndani ya kipindi cha miezi isiyozidi saba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni sehemu ya mapambano ya kujenga misingi ya uchumi kwa kudhibiti rushwa na mianya yake na kuleta uwajibikaji.
Akiahirisha Bunge jana mjini hapa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema utekelezaji wa ahadi hiyo unakwenda sambamba na kuonesha dhamira ya serikali ya kushughulikia makosa ya rushwa na kuweka misingi imara ya uwajibikaji katika sekta zote.
“Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kufanya uhalifu huo yaani kuwa deterrent,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa kuwapo kwake kutahamasisha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila shaka huku umuhimu kwao, ikiwa ni kulipa kodi.
Akielezea umuhimu wa mahakama hiyo, alisema kwamba itasaidia kuendeleza nia ya serikali ya watu kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment