Friday 18 November 2016

Jibu la TANESCO kuhusu kupandisha Bei ya gharama za umeme.


Naibu Mkurugenzi Mkuu (Usafirishaji Umeme) wa Tanesco, Kahitwa Bishaija alisema shirika hilo limelazimika kuwasilisha ombi la kupandisha bei ili kumudu gharama za uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kuboresha huduma kwa wateja. 

Alisema licha ya uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kuongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 58 mwaka huu, huku matumizi ya mafuta mazito kuzalisha umeme yakibakia asilimia tano pekee kulinganisha na asilimia 19 ya zamani, bado shirika hilo linakabiliwa na hali ngumu kiuendeshaji kutokana na madeni.

Alisema deni la Tanesco limeongezeka kutoka Sh699.57 bilioni Desemba mwaka jana hadi Sh794.48 Septemba na kwamba licha ya kuongeza mapato hadi kufikia Sh1,042.5 bilioni kulinganisha na Sh995.3 bilioni za mwaka jana, inalazimika kutumia wastani ya asilimia 13 ya mapato yake kwa mwezi kununulia mafuta ya kuzalisha umeme.

Bishaija aliwaeleza wadau kuwa ukokotoaji wa bei mpya inayoombwa umezingatia gharama ya ufuaji umeme, usafirishaji, usambazaji, uchakavu na uendeshaji.

Mhandisi kutoka Tanesco, Sophia Mgonja alisema ongezeko hilo la bei linatokana na ukame ulioikumba nchi kutokana na mvua kutonyesha kwa kiwango kinachotakiwa na kwamba kina cha maji katika Bwawa la Mtera ni kidogo hivyo wasipofanya juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia umeme, kutakuwa na mgawo.

“Pia kama mnavyofahamu kuwa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa umeshatabiri kuwa mwaka huu hakutakuwa na mvua za kutosha hivyo kama tusipofanya juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia umeme tunaweza kukwama huko mbeleni,” alisema Mgonja.

USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

                              SUBSCRIBE ON YOUTUBE TIKISA TV

No comments:

Post a Comment