Uongozi wa Klabu ya Singida United, umesema kuwa, wamepanga mechi zao za kwanza za nyumbani za Ligi Kuu Bara wachezee kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kutokana na uwanja wao wa Namfua kutokuwa tayari.
Mechi ambazo timu hiyo inaweza kucheza mkoani Dodoma ni dhidi ya Mbao iliyopangwa kupigwa Septemba Mosi pamoja na ile dhidi ya Stand United ambayo katika ratiba inaonyesha itachezwa Septemba 9. Mechi hizo zote zilitakiwa kupigwa katika Uwanja wa Namfua ambao bado upo kwenye matengenezo makubwa.
Katibu wa klabu hiyo, Abdulrahman Sima, amesema: “Uwanja wetu wa Namfua bado haujakamilika na sidhani kama ligi ikianza utakuwa tayari kutumika, marekebisho yanayofanywa ni makubwa, zile nyasi zilizopandwa zinaendelea kuota japo itakuwa haraka sana kuutumia.
“Kutokana na hali hiyo, tumeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ,kuturuhusu kuutumia Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma kwa mechi zetu za awali za nyumbani mpaka pale uwanja wetu utakapokuwa tayari na TFF wamekubali ombi letu.”
Timu hiyo ambayo imepanda daraja hivi karibuni, Agosti 26, mwaka huu itaanza mechi yake ya Ligi Kuu Bara ikiwa ugenini kucheza dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mwadui Complex
No comments:
Post a Comment