Manchester United walizidiwa nguvu na mabingwa wa Uhispania na Ulaya Real Madrid kwenye mechi ya Kombe la Super Cup la Uefa iliyochezewa Skopje, Macedonia chini ya joto kali.
Madrid walidhibiti mchezo huo kuanzia kipenga cha kwanza kilichopulizwa.
Walijipata kifua mbele pale Casemiro alipowafungia, muda mfupi baada ya kugonga mwamba wa goli.
Waliongeza la pili kupitia Isco aliyefunga akiwa hatua nane kutoka kwenye goli baada ya kubadilishana pasi na Gareth Bale, ambaye alichezeshwa safu ya mashambulizi badala ya Cristiano Ronaldo.
Mshambuliaji wa United aliyenunuliwa £75m Romelu Lukaku alikomboa bao moja lakini Marcus Rashford akapoteza fursa nzuri ya kufunga kwa kuutuma mpira nje.
Madrid wamekuwa timu ya kwanza kufanikiwa kutetea Kombe la Super Cup la Uefa tangu 1990.
Mechi hiyo ilichezewa katika uwanja chini ya joto kali la nyuzi joto 30C katika mji mkuu huo wa Macedonia.
Wachezaji walipewa muda mara mbili kupoesha joto, kama chini ya utaratibu wa Uefa.
Red Devils wametumia £146m majira ya joto kununua mshambuliaji wa Everton Lukaku (£75m), kiungo wa kati wa Chelsea Nemanja Matic (£40m) na beki wa Benfica Victor Lindelof (£31m) wakijaribu kujiimarisha baada ya kumaliza nambari sita ligini msimu uliopita.
Wachezaji hao watatu walichezeshwa na meneja Jose Mourinho dhidi ya Madrid.
Upande wa Madrid, ni Ronaldo pekee ambaye alikuwa hayupo kwenye kikosi kilichoanza mechi ukilinganisha na kikosi kilichocheza fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Juventus.
United walihangaika dhidi ya Madrid, hasa kipindi cha kwanza ambapo Madrid walitawala kwa kasi na pasi.
No comments:
Post a Comment