Baada ya kujisalimisha kituo cha polisi kwa wito wa Kamanda wa Polisi Dar es salaam , Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ameeleza kuwa sababu ya kupekuliwa nyumbani kwake ni kutafutwa kwa nyaraka za uchochezi.
Sheikh Ponda ambaye alishikiliwa na polisi kwa takriban siku mbili baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu safari yake ya Nairobi, Kenya alikokwenda kumjulia hali mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kwamba Polisi walifanya upekuzi nyumbani kwake Ubungo Kibangu lakini hawakufanikiwa kupata chochote.
”Kuhusu upekuzi uliofanyika nyumbani kwangu Ubungo - Kibangu, polisi walidai wanatafuta kama kuna nyaraka zozote za uchochezi, lakini hawakuzikuta". Amesema Sheikh Ponda
Aidha Kiongozi huyo ambaye pia ni Mwanaharakati wa haki za Waislamu amekanusha tuhuma kuwa alitoa maneno ya uchochezi alipozungumza na waandishi wa habari na badala yake, amesema alikuwa akitoa tahadhari kwa matukio yanayojitokeza na jinsi ya kuyakabili kwa mustakabali wa amani ya nchi.
“Nilizungumza kwa nia nzuri kwa masilahi ya Taifa na umma. Nilikuwa nakumbushia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwamba vina wajibu wa kusimamia amani na usalama. Kile nilichozungumza nimewaeleza nilikuwa sahihi na sikuwa na nia mbaya hata kidogo". Amefafanua
No comments:
Post a Comment