Yanga imefanya uamuzi wa kubadili upepo baada ya kubadili kambi yao kutoka Mwanza na kukimbilia Tabora kama ilivyokuwa kwa watani wao Simba walipojiandaa na mchezo dhidi ya Stand United.
Uamuzi huo wa Yanga ulichukua muda mfupi baada ya kutua Mwanza na kuamua kwenda Tabora kujiandaa na mechi dhidi ya Stand United njia ambayo iliyotumia na Simba na kufanikiwa kupata ushindi dhidi ya wapiga debe hao wa Shinyanga.
Akili hiyo sasa ndiyo iliyotumiwa na Yanga ambao jana alfajiri kikosi chao badala ya kuingia Mwanza kuweka kambi kwa muda ya kujiandaa kuwafuata Stand waliamua kubadili njia na kwenda Tabora.
Akizungumza hii leo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema wameamua kuweka kambi Tabora ikiwa ni maelekezo ya benchi la ufundi lililokubaliana na uongozi wa klabu hiyo.
Hafidh amesema wakiwa mkoani Tabora watakuwa na kambi hiyo fupi itakayoambatana na mchezo mmoja wa kirafiki kisha kurudi Shinyanga kuwafuata Stand.
"Tumekubaliana timu inakwenda kuweka kambi Tabora hayo ndiyo maamuzi ya mwisho yaliyotoka kwa uongozi na kuungwa mkono na benchi la ufundi," amesema Hafidh.
"Tunataka kupata sehemu itakayokuwa na utulivu ili tujiandae na huo mchezo muhimu kama unavyoona ligi ni mbichi, lakini pia ni ngumu lazima uwe na maandalizi ya maana kwa kila mchezo tukitoka huko tutarudi Shinyanga kucheza mechi yetu dhidi ya Stand."
No comments:
Post a Comment