Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe. Freeman Mbowe amesema kuwa hali ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu sasa imezidi kuimarika na kusema atasafirishwa kwa matibabu ya awamu ya tatu siku za karibuni.
Mbowe amesema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya chama hicho, alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya Tundu Lissu na kusema mpaka sasa Mbunge huyo anaendelea vizuri na kudai amefanyiwa upasuaji mara 17.
"Tundu Lissu mpaka sasa amefanyiwa upasuaji mara 17 amewekewa damu nyingi kuliko mgonjwa yoyote katika hospitali ya Nairobi lakini Mungu ameendelea kutenda miujiza kwake, saizi mashine zote zilizokuwa zinamsaidia zimeondolewa, saizi hapumulii mashine tena, mirija yote aliyokuwa anatumia kwa ajili ya chakula imeondolewa na juzi kwa mara ya kwanza aliweza kukaa" alisema Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA aliendelea kueleza kuwa "Matibabu ya awamu ya tatu ya Tundu Lissu yatafanyika nje ya nchi haitakuwa tena Kenya wala Tanzania, lakini kwa sababu za usalama hatuwezi kusema atakwenda sehemu gani au nchi gani, ukifika wakati sahihi tutasema hiyo awamu ya tatu ya matibabu itakuwa ya muda mrefu kidogo" alisema Mbowe
Mbali na hilo Mbowe ameendelea kusema kuwa serikali inafahamu watu ambao wameshambulia Tundu Lissu na kudai wao hawana imani na vyombo vya dola nchini na kusema vyombo hivyo vimekuwa tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo hawana nia ya dhati katika kufanya uchunguzi juu ya sakata la Tundu Lissu kupigwa risasi mnamo Septemba 7, 2017.
No comments:
Post a Comment