Friday 8 December 2017

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Ramadhani Madabida apelekwa Mahakama ya Mafisadi.

Image result for Ramadhani Madabida
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu kesi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kuhamishiwa Mahakama ya Mafisadi kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.


Madabida na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi ‘ ARV’s ‘ na kusababisha hasara ya Sh.Mil 148 ambayo ipo chini ya bilioni moja ambapo walifunguliwa kesi hiyo mpya namba 80 ya 2017, baada ya mahakama kuwafutia kesi kama hiyo iliyofunguliwa mwaka 2014.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Seif Shamte (mkurugenzi wa uendeshaji), Simon Msoffe (meneja masoko) na Fatma Shango (mhasibu msaidizi) wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa. ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kuisambazia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kopo 4476 za ARV.

Pia washtakiwa wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 98,506.08 (sawa na Sh 148,350,156 za Tanzania kwa udanganyifu baada ya kuonyesha kwamba fedha hizo ni malipo ya makopo 12252 ya dawa hizo za ARV’s.

Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa mbele ya hakimu Mkazi, Victoria Nongwa na Wakili wa Serikali, Pius Hilla Wakati ambapo upande wa utetezi wa watuhumiwa wanawakilishwa mawakili Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemiah Nkoko ambapo wakili wa utetezi, Msafiri alidai kuwa Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuisikiliza hiyo kwa sababu kiwango chake cha fedha kipo chini ya Sh.1 bilioni.

No comments:

Post a Comment