Tuesday 19 December 2017

Masharti aliyepewa na Mahakama Sadifa Juma baada ya kupewa dhamana.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Dodoma iemwachia kwa dhamana aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis (Mbunge) anayekabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa UVCCM Taifa.


Sadifa ameachiwa leo Desemba 19, 2017 baada ya mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa mashtaka ambao waliliwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai kuwa atavuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa UVCCM  ambao ulifanyika wiki iliyopita Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Mjini Dodoma.

Mtuhumiwa huyo ametakiwa kudhaminiwa na watu watatu pamoja na kusaini bondi ya Tsh. Milioni 1, huku akipewa masharti ya kutosafiri nje ya nchi.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo alidai Sadifa anashtakiwa kwa makosa mawili ambapo katika shtaka la kwanza Desemba 9,2017 katika makazi yake kwenye Kata ya Mnada, Mjini Dodoma akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM na mwajiri wa umoja huo aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.

Sadifa katika shtaka la pili anadaiwa katika eneo hilo na siku hiyohiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi huo.

Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga alipinga hoja ya kunyimwa dhamana mteja wake akisema makosa aliyoshtakiwa nayo mteja wake yana dhamana na hawezi kuingilia uchaguzi kwa kuwa umeshafanyika na mshindi ametangazwa.

Baada ya kuchambua hoja za pande zote Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo ameruhusu dhamana hiyo kwa Sadifa.

No comments:

Post a Comment