WAKATI zikiwa zimebaki siku tisa pekee kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, Kamati ya Usajili ya Yanga chini ya mwenyekiti wake, Hussein Nyika, muda wowote ule kutoka sasa inajipanga kumtambulisha mshambuliaji mpya ndani ya kikosi hicho ambaye atachukua mikoba ya Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye ameonekana kuwa msumbufu.
Yanga kwa sasa inatumia nguvu kubwa kwa ajili ya kusaka mshambuliaji mwingine wa kimataifa ambaye atakuja kuungana na washambuliaji, Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu kwa ajili ya kuimarisha safu yao hiyo.
Chanzo makini kutoka Yanga kimesema kuwa kwa sasa mwenyekiti wa kamati hiyo anajipanga kutambulisha mshambuliaji mpya ambaye anaweza kutokea Liberia, Burundi, DR Congo na Ghana ambapo hivi karibuni alipita kwenye nchi hizo kwa ajili ya kusaka mchezaji huyo.
“Muda wowote ule mkae mkao wa kula kwani kunaweza kukatokea jambo la kushangaza kwa kushushwa mshambuliaji mpya ambaye atakuja kuongeza nguvu kwenye eneo letu la ushambuliaji, ambapo mchezaji huyo ndiye atakuja kuchukua mikoba ya Ngoma ambaye yupo kwenye mstari mwekundu wa kuachwa.
“Atakayehusika na zoezi hilo ni mwenyekiti Hussein Nyika, ambaye hivi karibuni alikuwa anazunguka kwenye nchi hizo kuhakikisha kila kitu kinaenda vizuri na muda si mrefu mambo yote yatakuwa wazi,” kilisema chanzo hicho.
“Tayari hadi sasa nimeshatangaza wachezaji wawili, Fiston Kayembe na Yohana Nkomola na siku chache zijazo kabla ya dirisha kufungwa basi nitaweka wazi kila kitu chetu.
“Hao ambao wanazungumziwa muda si mrefu mtapata majibu yake kama watakuja hapa au la, lakini kwa sasa subirini.” alisema Nyika.
No comments:
Post a Comment