Baada ya kuituliza Singida United kwa bao 1-0 na kutinga fainali ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioba amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya fainali dhidi ya URA ya Uganda.
URA ya Uganda ndiyo ilianza kutinga fainali baada ya kuitoa Yanga kwa mikwaju 5-4 ya penalti ikiwa ni mara ya tatu wakiing’oa Yanga katika michuano hiyo tokea waanze kukutane.
Cioba raia wa Romania amesema wamejiandaa na sasa watakachofanya ni maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo huo wa fainali keshokutwa.
"Tumefika hapa kutokana na maandalizi na timu nzima kujituma, tunajua mechi ya fainali itakuwa ngumu zaidi kwa kuwa URA watakuwa na mbinu tofauti.
"Sisi tuko tayari na tutaendelea kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya mechi hiyo," alisema.
Azam FC ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano hiyo baada ya timu zote za Tanzania Bara na Visiwani, kung'olewa.
No comments:
Post a Comment