Beki wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael, juzi alikuwa shujaa wa timu hiyo kwa kufunga bao la umbali wa mita 25 katika mchezo dhidi ya Azam, kisha akafunguka kuwa aliamini atafunga bao hilo baada ya kumchungulia alivyokuwa amekaa golini, kipa wa Azam, Mghana, Razak Abarola.
Katika mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga ambao walikuwa wageni walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku wakivunja rekodi ya timu hiyo kutokufungwa kwenye ligi ya msimu.
Beki huyo amefunguka kuwa awali alipanga kutoa krosi kwa washambuliaji wa kati kabla ya kuamua kuupiga moja kwa moja baada ya kumchungulia kipa alipokuwa amekaa.
“Nilijua litakuwa bao kwa jinsi ule mpira nilivyokuwa nimeupiga kwa sababu awali kabla ya kupiga baada ya ile pasi nilitaka kutoa krosi lakini nilivyomuangalia kipa alipokuwa amekaa, nikaamua kuupiga moja kwa moja na matokeo yake likawa bao zuri.
“Nashukuru kwa kuweza kufunga haijalishi nacheza timu gani kwa sababu kama Azam nilikuwa nacheza zamani siyo sasa na ilikuwa lazima niipiganie timu yangu kuhakikisha inapata matokeo ya ushindi na ndiyo maana nilishangilia kwa kuwaambia mashabiki wa timu yangu kelele zao hatujasikia na sikuwa na maana nyingine,” alisema Michael.
No comments:
Post a Comment