Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amefunguka kuwa, amemuandaa ipasavyo beki wake Juma Nyosso kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Lipuli FC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kawaida Nyosso ambaye ni beki mzoefu hucheza namba tano au kitasa cha timu kuhakikisha hakuna hatari langoni mwake akishirikiana na Mohamed Fakhi, wote waliwahi kucheza Simba.
Jumatatu iliyopita, Nyosso alikumbana na kadhia baada ya kumshambulia shabiki wa Simba, Shabani Hussein (23) mfanyabiashara ndogondogo ambaye alizimia na kukimbizwa hospitali baada ya kumchokoza kwa kumpulizia vuvuzela sikioni.
Kufuatia tukio hilo, beki huyo alijikuta mikononi mwa polisi ambapo alilala siku moja kabla ya kuachiwa kwa dhamana siku ya Jumanne jioni.
Maxime alisema kuwa, beki wake huyo hana tatizo lolote la kushindwa kumtumia katika mchezo wake dhidi ya Lipuli na kudai kuwa atakuwa miongoni mwa wachezaji 11 watakaocheza mchezo huo.
“Nyosso hana matatizo yoyote ya kushindwa kumtumia katika mchezo wetu na Lipuli, hana jeraha lolote wala nini, ni mmoja wa wachezaji ninaowategemea katika kikosi changu.
“Shabiki ndiye alikuwa na makosa ya kumfuata mchezaji, mashabiki kama hao hawafai kwa kuwa wanafanya matendo ambayo si ya kiungwana,” alisema Maxime.
No comments:
Post a Comment