Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaanza kesho Jumamosi, lakini upande wa kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude amesema msimu huu ni lazima timu hiyo ichukue ubingwa kutokana na mambo makubwa ya kiufundi wanayoyapata kutoka kwa viongozi wao wa benchi la ufundi linaloongozwa na Mfaransa, Pierre Lechantre pamoja na Mrundi, Masoud Djuma.
Mkude alisema msimu huu Yanga itausikia mbali ubingwa wa ligi kuu kutokana na mbinu mbalimbali za kiufundi ambazo makocha hao wamekuwa wakiwapatia kila siku mazoezini.
Alisema mbinu hizo zimewasaidia kuwajenga kiakili na kistamina, hivyo hivi sasa wanajiamini zaidi wanapokuwa uwanjani lakini pia kuwa na uwezo wa kutafuta ushindi kwa njia yoyote ile bila ya kukata tamaa.
“Kwa hiyo msimu huu ni lazima tuchukue ubingwa wa ligi kuu ili mwakani tuweze kushiriki michuano ya kimataifa, hatuna njia nyingine ya kutufikisha huko baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la FA.
“Ubora wetu umeongezeka na tupo vizuri kila idara, ninawapongeza sana makocha wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” alisema Mkude.
No comments:
Post a Comment