Mabingwa wa Ulaya Ureno walipokezwa kichapo cha kushangaza na Uholanzi katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyochezewa mjini Geneva, Uswizi.
Winga wa zamani wa Manchester United Memphis Depay na mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Ryan Babel waliwaweka Waholanzi 2-0 mbele.
Beki wa Uholanzi Virgil van Dijk, ambaye majuzi alitawazwa nahodha mpya wa timu hiyo, alifunga la tatu.
Mchezaji wa Ureno Joao Cancelo alipewa kadi nyekundu dakika ya 61 baada ya kupokezwa kadi ya pili ya manjano.
Katika mechi hiyo, mkimbio wa kufunga mechi nane mtawalia wa mshambuliaji nyota wa Ureno anayechezea Real Madrid Cristiano Ronaldo ulifikishwa kikomo.
Nahodha huyo wa Ureno aliondolewa uwanjani dakika ya 68 na nafasi yake akaingia kiungo wa Monaco Joao Moutinho.
Ronaldo alikuwa amefunga mabao 17 akichezea Real na mawili akichezea Ureno dhidi ya Misri Ijumaa katika kipindi hicho alichofunga mabao mechi nane mtawalia.
Ureno wamo Kundi B katika Kombe la Dunia pamoja na Uhispania, Morocco na Iran.
Lakini Uholanzi, ambao walishindwa 1-0 na England mechi ya kwanza Ronald Koeman akiwa mkufunzi wao, hawakufuzu kwa michuano hiyo itakayoanza mwezi Juni.
No comments:
Post a Comment