Magoli 39.Magoli 11 katika mechi
saba za Borussia Dortmund. Magoli 10 katika mechi saba za Klabu Bingwa
Ulaya. Yote hayo akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Bila kusahau amefunga magoli matatu kwenye mechi moja (hat-trick) katika michezo sita.
Usiku wa Uefa Champion ligi, Haaland aliendeleza kasi yake kwa kupachika magoli mawili wakati timu yake ya Dortmund ikiifunga PSG 2-1 kwenye raundi ya kwanza ya mtoano wa Klabu Bingwa Ulaya.
Haaland ameweka rekodi ya kufikisha magoli 10 ya Klabu Bingwa Ulaya kwa haraka zaidi, baada ya kucheza mechi saba, rekodi iliyopita ilikuwa magoli 10 katika mechi 11.
Pia amekuwa mchezaji wa kwanza wa umri wa chini ya miaka 20 kufikisha magoli 10 katika Klabu Bingwa Ulaya katika msimu mmoja.
Kylian Mbappe, hakuliweza hilo na hata washambuliaji hatari wa zama hizi Cristiano Ronaldo na Lionel Messi hawakupata rekodi hizo wakiwa na umri wake.
Kwa taarifa yako tu, msimu huu wa 2019-20 Haaland ana magoli mengi zaidi kuliko kikosi chote cha Barcelona katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Haaland pia amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Dortmund kufunga katika mechi yake ya kwanza ya ligi ya Bundesliga, mechi ya kwanza ya Kombe la Ujerumani na mechi ya kwanza ya Klabu Bingwa Ulaya.
Na kwa sasa kinda huyo ni kinara wa magoli katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa sawa na mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski.
Robert Lewandowski. |
Lakini pamoja na yote hayo, Haaland wala si mtu wa majivuno.
"Nafurahi kupata tuzo ya mchezaji bora, lakini naamini naweza kufanya zaidi ya hapa," amesema baada ya mechi ya jana usiku na kuongeza: "Inanipasa nicheze vizuri zaidi kwenye kiwango hiki, niongeze bidii zaidi."
"Matokeo haya bado ni ya hatari kwetu, PSG wana kikosi kikali na wanaweza wakapita katika raundi ya pili. "
Toka alipojiuga na Dortmund mwezi Januari, ameshafunga magoli 11 katika dakia 450 alizocheza - sawa na wastani wa goli moja katika kila dakika 41.
Ni wachezaji 11 tu ambao wanamzidi magoli katika ligi ya Bundesliga msimu huu, japo Haaland amejiunga katikati ya msimu na kucheza mechi tano tu.
Alinyakua tuzo ya mchezaji bora wa Bundesliga kwa mwezi Januari - licha ya kucheza chini ya saa moja tu katika mwezi huo.
Mshambuliaji huyo kinda wa timu ya taifa ya Norway alikuwa akihusishwa na kuhamia katika klabu za Man United na Juventus mwezi uliopita lakini akajiunga na Dortmund akitokea Red Bull Salzburg kwa dau la Euro milioni 20m.
Kabla ya uhamisho huo, Haaland alikuwa ameshaifungia Slazburg magoli nane kwenye Klabu Bingwa Ulaya katika mechi sita za hatua ya makundi.
Siku za nyuma asingeruhusiwa kuiwakilisha Dortmund kwenye michuano hiyo, lakini msimu uliopita Uefa walibadili kanuni kuruhusu mchezaji kuweza kuchezea klabu mbili kwenye msimu mmoja wa Klabu Bingwa.
"Yeye ni mpachika magoli, ana miaka 19 tu, ni kipaji kikubwa alichonacho," anaeleza mchezaji mwenzake wa Dortmund Axel Witsel.
"Bado ana nafasi kubwa ya kuimarika na yumo njiani kuwa mchezaji mkubwa sana."
Haaland, alizaliwa Leeds Uingereza wakati baba yake Alf-Inge Haaland, alipokuwa akicheza nchini humo akianzia Leeds United kisha Manchester City.
No comments:
Post a Comment