Tuesday 26 April 2016

Baada ya Bilioni Mbili za Maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano kuhudumia wananchi,Rais Magufuli atoa msamaha kwa wafungwa


Rais Dk.John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa wote kwa kuwapunguzia 1/6 ya vifungo vyao huku wafungwa 3,551

wakifaidika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ambao kati yao 580 watachiliwa huru na 2,971 wanabaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Rais Magufuli ametoa msamaha huo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 42 ya muungano kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45(1)(d) ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ambao utawahusu wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu, na kansa ambao wako kwenye hatua za mwisho, wafungwa waliothibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi ambao umri huo umethibishwa na jopo la waganga, wafungwa wakike walioingia na mimba gerezani na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya pamoja na wenye ulemavu wa mwili na akili ambao pia wamethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Msamaha huo hautawahusu waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa ama kifungo cha maisha, makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya,uombaji na upokeaji rushwa, unyang’anyi kwa kutumia silaha, makosa ya kupatikana na silaha, risasi na milipuko isiyo halali.

Wengine ni wale wanaokabiliwa na makosa ya shambulio la aibu, ubakaji, kunajisi na kulawiti, wenye makosa ya kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliotenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, wizi wa magari, pikipiki, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Waliohukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino, usafirishaji wa nyara za serikali na ujangili,wizi/ubadhilifu wa fedha za serikali, kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulizi halali na wale walioingia gerezani baada ya tarehe 26/02/2016.

No comments:

Post a Comment