Friday, 22 April 2016

Michuano ya vijana kufanyika nchini India Serengeti Boys kuanza na Marekani.

Timu ya taifa ya vijana ya umri wa miaka chini ya 17 Serengeti Boys inataraji kufungua dimba na Marekani katika mchezo wa kwanza wa michuano ya vijana itakayofanyika nchini India kuanzia Mei 15 mwaka huu na siku 2 baadae watavaana na wenyeji India.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini India (AIFF) limetoa ratiba ya michuano ya vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) itakayoanza kutimua vumbi Mei 15 -25 katika mji wa Goa nchini India kwa Serengeti Boys kufungua dimba na Marekani.
Michuano ya AIFF inashirikisha timu tano za vijana wenye umri chini ya miaka 17 kutoka nchi za Korea Kusini, Marekani, Malysia, Tanzania na wenyeji India.
Mashindano hayo yatafanyika katika uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa kuanzia Mei 15, ambapo Tanzania itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Marekani, huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia.
Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utchezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.
Kikosi cha Serengeti Boys kianatarajiwa kuingia kambini mwishoni mwa mwezi Aprili, 2016 kujiandaa na michuano hiyo ya vijana na kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 mwakani nchini Madagascar.

No comments:

Post a Comment