Saturday, 14 May 2016

Jumuiya ya Madola Kuiga Mbinu za Tanzania Katika Kupambana na Rushwa.

waziri
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa amesema Jumuiya ya Madola inaweza kuiga mbinu ambazo Tanzania imetumia katika kupambana na rushwa zikiwemo za kujumuisha wadau tofauti kwenye vita hiyo.

Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bibi Patricia Scotland walipokutana kwenye mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.

Amemweleza Katibu Mkuu huyo kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupambana na rushwa kutokana na ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka kwa wananchi.

Waziri Mkuu alitoa wito huo baada ya kuelezwa na Bibi Scotland kwamba anataka kuanzisha idara malum kwenye Jumuiya hiyo ambayo itasimamia mapambano dhidi ya rushwa na makosa ya jinai.

Amesema ameamua kufanya hivyo ili aweze kuendanana na malengo makuu matatu ya jumuiya hiyo ambayo ni kupiga vita rushwa, kuhimiza utawala bora na usimamizi wa demokrasia.

No comments:

Post a Comment