Tuesday 17 May 2016

Klabu ya Yanga tayari imewasili mjini Dundo nchini Angola.

 
Yanga SC imewasili salama mjini Dundo, Angola baada ya safari ya kutwa nzima, tayari kwa mchezo wao wa kesho dhidi ya wenyeji, Sagrada Esperanca kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya kutua Luanda, Yanga iliunganisha ndege nyingine kwenda Dundo ambako ni maskani ya Sagrada Esperanca.

Katika mchezo wa kesho, Yanga itahitaji sare ili kuingia hatua ya makundi, baada ya awali kushinda 2-0, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony wiki iliyopita Dar es Salaam.

Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema ana imani kurejea kwa wachezaji wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma kutaiogezea nguvu timu yake. 

Wawili hao waliukosa mchezo wa kwanza kutokana na kuwa wanatumikia adhabu ya kadi za njano walizopewa kwenye mechi mfululizo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwezi uliopita Dar es Salaan na Cairo, Yanga ikitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini.

Mechi ya kesho itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.

Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.

Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.

No comments:

Post a Comment