Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 26 Novemba, 2016 ametunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 194 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kundi la 59/15 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni nje ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kilichopo mkoani Arusha, na ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni ndani ya Ikulu.
Maafisa hao ambao 168 ni wanaume na 26 ni wanawake, wametunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu na sasa wamekuwa Maafisa Wapya wa JWTZ.
Kabla ya kutunuku Kamisheni, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Maafisa wanafunzi wa JWTZ na baadaye akashuhudia uhodari wa askari kutoka kikosi cha maadhimisho cha JWTZ waliofanya onesho la gwaride la kimyakimya.
Akizungumza baada ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Makamanda na Askari wote wa JWTZ kwa jukumu kubwa wanalolitekeleza la kuhakikisha nchi ipo salama na amesema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi maslai na mazingira ya kazi kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Aidha, Rais Magufuli amesema ameamua tukio hili la kutunuku Kamisheni lifanyike Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa heshima kwa Maafisa wa JWTZ kama ambavyo Viongozi wengine Serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa Ikulu.
"Kwamba Mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, Wakuu wa Mikoa tunawaapishia hapahapa, Makatibu Wakuu tunawaapishia hapahapa, kwa nini hawa Maafisa wa Jeshi tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? Nyinyi ndio mnalinda nchi, nyinyi ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine mpaka wamekuwa Mabrigedia Jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni kwenu" amesema Rais Magufuli.
Sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi hao zimehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi wastaafu na Majenerali wastaafu wa JWTZ.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
26 Novemba, 2016
USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment