MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi ametetea kauli ya Rais John Magufuli kuhusu kufanya siasa wakati huu na kwamba alichotaka kiongozi huyo wa nchi ni ushirikiano kutoka kwa wanasiasa wenzake ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema Rais Magufuli, katika kauli yake ile hakumaanisha kuzuia shughuli za siasa nchini isipokuwa alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona siasa zinakwamisha mikakati ya kuwapelekea wananchi maendeleo yao.
Jaji Mutungi alisema hayo Dar es Salaam jana, alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka watu kuacha siasa za hovyo hadi mwaka 2020 utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine, ili muda uliopo wautumie kuijenga nchi.
“Watu wametafsiri tofauti kauli ya Rais, lakini ni kwamba alikuwa akiomba ushirikiano wa wanasiasa wenzake na wadau wote wa siasa kuleta maendeleo… kwa hiyo kabla ya kukosoa kauli ni vyema ukafanya utafiti siyo kuibeba na kuitafsiri kwa mrengo tofauti,” alisema .
Alisema siyo kwamba Rais anapinga siasa isipokuwa anapingana na wanasiasa ambao ni pingamizi katika kuleta maendeleo na muda wote wamejikita katika siasa bila kuangalia namna ya kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Alisema wapo watu walioitafsiri tofauti hotuba aliyoitoa juzi Rais Magufuli, hivyo wananchi wanapaswa kuwa watafiti na kuweka maslahi ya nchi huku akiwataka wanasiasa kuwa wavumilivu na kutumia muda wao kutafakari jambo kabla ya kuzungumza.
“Rais alikuwa akijaribu kuwasihi wanasiasa kuangalia namna ya kujikita kwenye siasa ya maendeleo ya jamii kwa ujumla na kuachana na siasa za kupinga maendeleo,” alisema.
Alisema dhamira ya Rais ni kuwaletea maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na vyama vinapaswa kufuata utaratibu wa kuwasilisha taarifa kwa msajili na si kusubiri hadi vyombo vya habari kutoa taarifa.
No comments:
Post a Comment